Dalili Na Tiba Ya Mfadhaiko (DEPRESSION)



Dalili Na Tiba Ya Mfadhaiko (DEPRESSION)

 

Maana Ya Mfadhaiko Wa Akili (Depression)


Kila mmoja wetu ameshapata kuwa na huzuni wakati fulani, ni kitu cha kawaida kinachotokea wakati umepotelewa na kitu, kutokana na mihangaiko ya maisha au kutokana na kudharauiliwa. Huzuni ikizidi na ikienda kwa siku nyingi mfululizo (wiki mbili au zaidi) na ikiambatana na hali ya kujiona kuwa si wa thamani tena, kwamba ni mtu usiye na msaada wo wote – basi hii inaweza kuwa ni zaidi ya huzuni. Unaweza kuwa umepata tatizo la kiafya – mfadhaiko, ugonjwa ambao kwa bahati nzuri una tiba.
Mfadhaiko ni ugonjwa unasababisha mtu kuwa na huzuni kila wakati na kukosa hamu ya kufanya vitu au kutenda yale aliyopenda sana kufanya zamani. Mfadhaiko ni ugonjwa unaoathiri namna mtu anavyojisikia, anavyofikiri na tabia yake.
Chanzo halisi cha ugonjwa huu bado hakijafahamika. Wataalamu wanasema kuwa ni muunganiko wa sababu nyingi ikiwa ni pamoja na urithi, mazingira ya maisha, mambo ambayo mtu amekutana nayo katika maisha na sababu za kisaikolojia. Mtu anaweza kukutana na jambo moja tu kubwa na baya katika maisha yake kama kufiwa na mtu wa karibu, mahusiano mabaya ya ndoa ua kubakwa na akapata mfadhaiko.
Mtu mwenye mfadhaiko hupungukiwa uwezo wake wa kutenda kazi kiasi kwamba yeye na walio karibu naye wote huathirika.
Ugonjwa huu huwapata zaidi watu wanaokunywa sana pombe au kutumia madawa ya kulevya. Watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, wenye magonjwa ya moyo, waliopatwa na kiharusi, wenye kansa, kisukari, ugonjwa wa Parkinson’s na baadhi ya magonjwa mengine huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na mfadhaiko. Mtu mwenye mfadhaiko pamoja na magonjwa hayo mengine huwa kwenye hali mabaya zaidi ya kiafya na hupata shida zaidi kuutibu ugonjwa huu.
Utafiti wa zamani ulisema kuwa watu wenye matatizo ya mfadhaiko waliathirika kutokana na kutengwa na jamii, lakini utafiti wa hivi karibuni umetoa majibu tofauti na kuonyesha kwamba mtu anatengwa na jamii kutokana na mfadhaiko alio nao.
Mfadhaiko ni ugonjwa ambao umefahamika toka zamani sana. Hippocrates aliuita ugonjwa huu Melancholia.
Watu wengi mashuhuri wameumwa ugonjwa huu na wengine katika maisha yao yote. Abraham Lincoln, raisi wa 16 wa Marekani na Winston Churchil wa Uingereza ni baadhi ya watu walioumwa ugonjwa huu katika maisha yao yote.

Aina Za Mifadhaiko Wa Akili


Tatizo hili la kuwa na mfadhaiko linakuja kwa namna nyingi. Hapa chini ni baadhi ya aina za mfadhaiko:
Major depressive disorder (major depression)
Mgonjwa mwenye aina hii ya mfadhaiko anakuwa na mchaganyiko wa dalili nyingi za mfadhaiko ambazo zitamfanya ashindwe kulala, kusoma, kufanya kazi, kula na kufaidi vitu ambavyo awali vilikuwa vinamvutia sana. Aina hii ya mfadhaiko humpotezea kabisa mgonjwa uwezo wa kushiriki kwenye shughuli za kazi vizuri. Watu wengine hupatwa na hali hii mara moja wakati wengine hurudiwa mara nyingi.
 Dysthymic disorder (dysthymia)  
Mgonjwa wa aina hii ya mfadhaiko anaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda mrefu, pengine miaka kadhaa, lakini hana dalili ambazo ni kali sana kama za aina ya kwanza hapo juu. Mgonjwa hufanya kazi zake ingawa si kwa ufanisi mkubwa na huwa si mtu mwenye raha kamili. Watu wengine hupatwa na hali hii mara moja tu katika maisha yao wakati wengine hurudiwa mara nyingi. Mgonjwa wa aina hii ya mfadhaiko huweza kupatwa na aina ya kwanza hapo juu mara moja au zaidi katika maisha yake.
  Psychotic depression
Endapo mfadhaiko utakuwa mkubwa na kuambatana na mtu kuwa na maluweluwe (hallucinations) na kuwa nje ya maisha halisi, mtu huyu anaweza kuwa na aina ya mfadhaiko unaoitwa Psychotic depression, ugonjwa ambao mara nyingine huitwa delusional depression.
Postpartum depression (postnatal depression)
Kama mama mzazi atapatwa na mfadhaiko wiki chache baada ya kujifungua, anaweza kuwa amepatwa na postnatal depression. Wataalamu wanasema kuwa asilimia 15 hadi 20 ya akina mama hupatwa na ugonjwa huu baada ya kujifunga, bahati mabaya ni kwamba wengi hawagunduliki na wanateseka kwa miaka mingi baada ya kujifungua. Mama anaweza kuupata ugonjwa huu muda wo wote katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kujifungua.
SAD (seasonal affective disorder)
Idadi ya watu wanaopatwa na ugonjwa huu huoongezeka zaidi kadiri unavyokwenda mbali zaidi na Ikweta. Mwisho wa kipindi cha summer ni mwanzo wa kuona jua kwa muda mfupi zaidi au mwanzo wa saa nyingi zaidi za giza kwa siku. Mtu anayepatwa na mfadhaiko katika kipindi hiki huweza kuwa amepeta aina hii ya ugonjwa. Ugonjwa huu hutoweka wenyewe wakati wa spring au summer.
Bipolar disorder (manic-depressive illness)
Ugonjwa hauonekani kwa wingi kama aina nyingine za hapo juu. Tabia kuu ya aina hii ya mfadhaiko ni kuwa na vipindi vya dalili kuwa juu sana na baadaye kushuka. Viwango hivi vya juu na chini huitwa manias.

Dalili Za Kuwa Na Mfadhaiko


  • Kutopenda kushirikiana na watu wengine
  • Kuwa na huzuni kila wakati na kujiona kuwa ni mtu usiyefaa
  • Kukosa mwamko na hamu ya kufanya shughuli
  • Matatizo katika kufanya maamuzi
  • Kutotulia na kuwa na hasira
  • Kula zaidi au pungufu ya kawaida
  • Kulala zaidi au pungufu ya kawaida
  • Kushindwa kutuliza mawazo kwenye jambo
  • Matatizo ya kumbukumbu
  • Kutotulia na kuwa na hasira
  • kukosa raha ya maisha
  • Kukosa hamu ya kufanya mambo uliyoyapenda sana zamani na  hamu ya kufanya mapenzi
  • Kujisika vibaya juu yako au kuwa mwenye makosa
  • Kuona kwamba huwezi kutatua matatizo yako ya maisha
  • Kuumwa kichwa, kubanwa misuli, matatizo ya uyeyushaji chakula tumboni, matatizo ambayo hayaponi kwa kutumia dawa
  • Kuwa na mawazo ya kujiua


Namna Ya Kuondoa Mfadhaiko


Kwa mtazamo wa haraka haraka unaweza kufikiria kuwa hakuna njia ya kukabiliana na msongo wa mawazo kwa sababu hata iweje bili za umeme na maji zitazidi kuja, siku ndiyo ile ile ya saa 24 na kazi za kufanya zinazidi kuwa nyingi na majukumu ya familia yatazidi kuongezeka. Ukweli ni kwamba una uwezo wa kumudu kuukabili msongo wa mawazo kuliko unavyojifikiria. Kuelewa kuwa majukumu haya yote ni ya kwako na kuwa wewe ndiye mtu pekee wa kuyaweka sawa, ndio msingi wa kuanza kukabiliana na msongo wa mawazo. Kukabiliana na msongo wa mawazo kunataka uamuzi wa kuanza kuchukua hatua kimawazo, kihisia na kwa kujiwekea ratiba na hatua nyingine za kukabiliana na matatizo yako.

Kubaini Vyanzo Vya Msongo Wa Mawazo


Hatua ya kwanza kabisa ni kubaini vyanzo vya msongo wa mawazo katika maisha yako. Kazi hii siyo rahisi sana kwa sababu vyanzo hivi huwa sio vya wazi na ni rahisi kudharau mawazo, hisia na tabia ambavyo huwa ndiyo mwanzo wa kukupa msongo wa mawazo. Kwa mfano, unawezajua fika kuwa mara nyingi huwa upo katika wasiwasi mkubwa wa kukamilisha kazi ulizopangiwa katika muda uliopewa, lakini usijue kuwa tabia yako ya kuahirisha kazi ndiyo tatizo na si ukubwa wa kazi unazopewa.
Kubaini ni nini vyanzo vya msongo wa mawazo kwako, chunguza kwa ukaribu sana tabia, mwenendo na visingizio vyako. Kama hutokubali kuwa wewe mwenyewe ni mhusika katika kusababisha na kuvilea vitu vinavyokuletea msongo wa mawazo (Stressors), itakuwa vigumu sana kupamabana na tatizo lako la kuwa na msongo wa mawazo.
Andaa kijitabu kubaini ni nini kinakuletea msongo wa mawazo na vipi huwa unakabiliana na hali hiyo. Kila wakati utakapopatwa na msongo wa mawazo, fuatilia kwa kutumia kijitabu chako. Ukifanya hivyo kila siku, utajifunza ni mambo gani yanakusumbua na yanavyohusiana. Katika kijitabu chako andika yafuatayo:
  • Ni nini kilisababishia msongo wa mawazo
  • Nilijisikiaje, kimwili na kihisia
  • Ulifanya nini kilipotokea
  • Ni hatua gani ulichukua kurudi kwenye hali yako ya kawaida

Chunguza Namna Unavyokabili Msongo Wa Mawazo


Ni muhimu sana kujua jinsi unavyokabiliana na msongo wa mawazo. Kama uliandika vizuri kijitabu chako, kitakupa picha nzuri ya jinsi unavyokabiliana na msongo wa mawazo. Njia nyingine ni nzuri na nyingine ni mbaya na kwa bahati mbaya watu wengi hukabiliana na tatizo hili kwa kutumia njia ambazo huongeza tatizo na si kulipunguza.

Njia mbaya za kuondoa msongo wa mawazo
Hebu tazama njia ambazo baadhi ya watu hutumia, njia ambazo hupunguza tatizo kwa muda mfupi na kulifanya tatizo kuwa kubwa zaidi baadaye:
  • Kuvuta sigara
  • Kunywa pombe sana
  • Kula sana au kula kidogo
  • Kukaa kwenye TV au kompyuta, saa nyingi sana
  • Kujitenga na marafiki, familia na shughuli
  • Kutumia vidonge
  • Kulala sana
  • Kuahirisha mambo
  • Kujishughulisha saa zote kuepuka matatizo
  • Kuwatulia wengine msongo wao (kubwatuka, kufoka, kupigana)
Jifunze njia nzuri za kuondoa msongo wa mawazo
Sasa chukua nafasi hii kujifunza baadhi ya njia nzuri ambazo unaweza kuzitumia kukabilina na msongo wa mawazo. Kuna njia nyingine nyingi tu lakini zote zinakudai uanze kufanya mabadiliko kimatendo. Kwa sababu kila mmoja wetu yupo tofauti na atakichukulia tofauti kinapotokea kitu cha kusababisha msongo wa mawazo, hakuna namna moja tunayoweza kusema ufanye linapotokea jambo fulani, hivyo basi itabidi ufanya utafiti na kuona ni njia zipi zinaleta mabadiliko kwako. Zingatia kile unachokimudu na utakochoona kuwa kinachokusaidia.
Kimsingi kuna njia kuu mbili; kubadili mazingira ya chanzo cha msongo ambapo unaweza kukikwepa au kukibadilisha na pili kubadilisha jinsi hatua unazochukua ambapo unaweza kubalika ili uendane nacho au kukabaliana nacho. Tutazielezea njia hizo za kuukabili msongo wa mawazo hapa chini:

1. Kukwepa Vyanzo Vya Msongo Wa Mawazo: 


Si rahisi kukwepa kila chanzo cha msongo wa mawazo na ni vibaya kukwepa chanzo cha msongo wa mawazo ambacho inabidi ukikabili. Ukiwa makini utashangaa kuona uwingi wa vyanzo vya msongo ambavyo unaweza kuvikwepa.
Jifunze kusema hapana: Tambua uwezo wako wa kimwili na kikazi na zingatia kufanya kazi kulingana na uwezo ulio nao. Kuchukua majukumu zaidi ya uwezo ni chanzo cha kujipa msongo wa mawazo.
Wakwepe watu wanaoklsababishia msongo: Kama kuna mtu anakusababishia msongo wa mawazo kila wakati, punguza muda wa kukutana naye au vunja kabisa mahusiano naye.
Dhibiti mazingira mabovu: Kama habari za jioni za kwenye TV zinakukera, zimisha hiyoTV na kama msongamano wa magari kwako ni kero, chukua njia nyingine isiyo na msongamano hata kama ni ndefu zaidi.
Kwepa mada zinazokupa maudhi: Kama mada za dini au siasa hukupa maudhi, acha kushiriki kwenye mada hizo. Kama kila siku unalumbana na watu fulani kuhusu mada fulani, acha kuanzisha mada hizo au tafuta kisingizio cha kuondoka mada hizo zinapoanzishwa.
Chunguza ratiba yako: Itazame kwa kina ratiba yako, majukumu yako na kazi ulizojipangia kwa siku. Kama mambo ni mengi mno, yagawanye kwenye makundi ya yale ambayo ni lazima yafanywe na yale ambayo ni muhimu kufanyika. Yale ambayo si ya lazima sana yaweke chini kabisa kwenye ratiba au yaondoe kabisa.

2. Badili Mazingira ya chanzo: 


Kama inashindikana kukwepa chanzo cha msongo wa mawazo, badilisha mazingira yake. Jaribu kufikiria ni nini cha kufanya ili chanzo hicho kisijitokeze tena hapo baadaye, hii inamaanisha kubadili namna yako ya mawasiliano au namna unavyoendesha shughuli zako.
Onyesha hisia zako: Kama kuna kitu au mtu anakukera, mweleze wazi kabisa kwa njia ya kistaarabu. Kama husemi, unajenga chuki na kuiacha hali ikibaki pale pale.

Usilee matatizo: Usilikalie lile linalokukera, liseme wazi na chukua hatua mara moja ya kulizuia. Kama una kazi muhimu ya kufanya na rafiki yako mpenda hadithi anaingia, mwambie wazi kuwa una kazi muhimu na kwamba unampa dakika kadhaa tu za mazungumzo.
Tumia muda wako vizuri: Kushindwa kutumia muda wako vizuri ni chanzo kikubwa cha kupata msongo wa mawazo. Unapokuwa umechelewa kukamilisha jambo lako, utalifanya bila utulivu na utakosa umakini. Lakini ukiwa na mpango mzuri wa muda wako, utafanya kila kitu mbele yako kiufanisi na bila kupatwa na msongo wa mawazo.

3. Badilika Kuendana Na Chanzo: 


Kama huwezi kukibadili chanzo cha msongo wa mawazo, wewe badili mtazamo wako kuhusu chanzo hicho:
Kitazame chanzo kwa mazuri yake: Kitazame chanzo cha kero         kwako kwa kutazama mazuri ambayo yanaweza kupatikana             kutokana na chanzo hicho. Badala ya kulalamika na kukasirika         kutokana na foleni ya magari, chukulia kuwa huo ndio muda mwafaka kwako kujipumzika au kusikiliza muziki unaaoupenda ndani ya gari yako.
Kuwa na mtazamo wa jumla: Litazame jambo linalokukera kisha         jiulize kama ni jambo litakalokusumbua kwa muda gani, mwezi             mmoja, mwaka na jee mwisho wa siku ni madhara gani                               yatakayotokea. Kama ni suala la mpito tu, elekeza nguvu zako               kwenye mambo mengine.
Rekebisha viwango vyako: Moja ya sababu ya kujipa msongo wa         mawazo ni kutaka kila kitu kiende sawa kwa kiwango cha hali ya           juu. Usijiweke kwenye mtego wa kushindwa kwa kujiwekea                   viwango vya juu kiufanisi. Jiwekee viwango vinavyowezekana kwako na kwa  wenzako na jifunze kukubali matokeo ambayo                 hayakufika kiwango lakini siyo mabaya.
Yakumbuke mazuri yako: Msongo wa mawazo ukikunyemelea,           chukua muda kidogo kushukuru kwa yale yaliyo mazuri katika               maisha yako, ikiwa ni pamoja na vipawa nyako vizuri na vyenye             nguvu. Hili litakusaidia kukupa mtazamo tofauti wa mambo yaliyo       mbele yako.

 4. Kubaliana Na Yale Ambayo Huwezi Kuyakabili: 


Vyanzo vingine vya msongo wa mawazo huwezi kuvibadili wala kuvizuia. Huwezi kukizuia kifo cha mtu wa karibu yako, wala ugonjwa mkubwa, au mporomoko wa uchumi wa nchi. Hapa inafaa kukubaliana na hali ingawa ni vigumu, lakini ni bora kuchukua msimamo huo kuliko kugombana na kitu usichoweza kukibadili.
Usijaribu kudhibiti kisichowezekana: Vitu vingi sana katika maisha yetu vipo nje ya uwezo wetu – hasa tabia za watu wengine. Kuliko kung’anga’nia na kugombana nao wabadili tabia, fikiria zaidi namna unavyoweza kuepukana na matatizo yao.
Tazama upande wa pili: Unapokumbana na vikwazo vikubwa, chukulia kuwa ni nafasi ya kujifunza na kukomaa. Kama ni maamuzi yako mwenyewe ndiyo yaliyokusababishia matatizo, chukua nafasi hiyo kutafakari na kujifunza kwa maamuzi yako ya baadaye.
Jifunze kusamehe: Lazima ukubali kuwa tunaishi katika ulimwengu wenye mapungufu mengi na kwamba binadamu kufanya makosa ni kawaida. Usiwe na hasira na chuki, jifunze kusamehe na kuendelea na mambo mengine.

5. Pumzisha Na Burudisha Mwili Wako


Mwili wako utapata uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na msongo wa mawazo endapo utaulea kwa kupata muda wa kuupumzisha na kuuburudisha. Katika kuulea mwili wako unaweza kufanya yafuatayo:

  • Fanya matembezi
  • Pumzika kwenye bustani au sehemu zenye mazingira ya asili
  • Mkaribishe rafiki nyumbani
  • Pata kikombe cha chai au kahawa
  • Jishughulishe kwenye bustani
  • Soma kitabu kizuri
  • Sikiliza muziki
  • Angalia vichekesho
  • Cheza na mnyama uliyemfuga

Kuulea mwili ni jambo la lazima na si jambo la kujifurahisha tu. Katika kuyafanya hayo, jipangie kabisa ratiba yako na usimruhusu mtu au vitu vingine kuvuruga ratiba yako, huu ni muda wako wa kuurudishia nguvu mwili wako. Jichanganye na marafiki wenye mawazo mazuri, hao watakusaidia kuondokana na madhara yanayotokana na kuwa na msongo wa mawazo. Jaribu kuwa ni mtu wa kufurahisha na kufurahia mambo kwani kicheko ni dawa ya kuondoa msongo wa mawazo kwa njia nyingi.

6. Mazoezi Na Chakula Kizuri


Unaweza kuongeza uwezo wako wa kukabiliana na msongo wa mawazo kwa kujenga afya ya mwili wako.

  • Fanya mazoezi
  • Kula chakula kizuri
  • Punguza matumizi ya kahawa na sukari
  • Acha sigara, pombe na madawa
  • Pata usingizi wa kutosha

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.