Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 06

Nikakata simu na kumfuta yule
kijana wa bodaboda.
“Shilingi ngapi?” nikamuuliza.
“Ni elfu mbili tu”
Nikatoa noti za shilingi elfu mbili
na kumpa.
“Baadaye nitakupigia uje
unichukue, sawa?”
“Itakuwa saa ngapi?”
“Sijajua lakini haitakuwa saa nyingi
sana”
“Sawa”
Kijana akaondoka na pikipiki na
kuniacha pale pale. Nilisimama kwa
dakika kadhaa huku nikitazama
kila upande kwa tamaa ya
kumuona yule msichana. Nilipoona
muda unazidi kwenda nikampigia.
“Nimekuchelewesha?” akaniuliza.
“Naona muda unazidi kwenda sioni
mtu”
“Sasa sikiliza nikwambie, fuata hiyo
njia ya miguu iliyoko nyuma ya
huo mbuyu uje moja kwa moja.
Mbele yako utakuta mwembe,
utakata kushoto…”
SASA ENDELEA
“Si uliniambia utanifuata hapa?”
nikamuuliza.
“Ndiyo lakini kuja huko
nimeshindwa, mwenzko naogopa.
Lakini wewe mwanume unaweza
kuja tu”
“Kwani wewe uko wapi?”
“Niko huku nilikokuonesha”
Nikatupa macho katika eneo hilo
lilioko nyuma ya ule mbuyu.
Niliona pori tupu.
“Kwani kuna nyumba huko?”
“Ziko nyingi tu”
“Ngoja nije”
“Njoo, nikikuona nitakufuata”
Nikakata simu na kwenda nyuma
ya ule mbuyu. Nikaona njia ya
miguu iliyoelekea kwenye pori.
Halikuwa pori la kutisha bali
lilikuwa la miti ya mikoroshi na
nyasi. Nikaifuata ile njia.
Nilikwenda taratibu huku
nikiangaza macho mbele ya lile
pori.
Kitu kilichonipa matumaini ya
kuwepo na nyumba ni kwamba
nilipishana na watu wawili
waliokuwa wakitoka katika eneo
hilo. Nilikwenda hadi nikauona ule
muwembe. Kulikuwa na njia
upande wa kulia na upande wa
kushoto wa muwembe huo.
Nikakumbuka msichana aliniambia
nishike njia ya upande wa kushoto.
Nikashika njia hiyo. Baada ya
kupiga hatua kadhaa nilianza
kuona nyumba moja moja.
Nyingine zilikuwa zimekamilika,
nyingine zilikuwa bado.
Msichana akanipigia simu,
nikaipokea.
“Nimeona mtu anakuja, sijui ni
wewe?” akaniuliza.
“Labda ni mimi kwa sababu niko
peke yangu”
“Umevaa tisheti nyekundu?”
“Ndiyo”
“Basi ni wewe, ngoja nikufuate”
“Kwa hiyo nikusubiri hapa nilipo au
niendelee?”
“Njoo tu na mimi ninakuja.
Tutakutana”
Msichana akakata simu.
Nikaendelea kwenda. Mara nikaona
msichana anakuja mbele yangu.
Alikuwa amevaa dera la mauaua.
Nikahisi alikuwa ndiye yeye.
Alipofika karibu yangu nikasimama,
akaja akasimama mbele yangu.
“Nafikiri wewe ni mgeni wangu”
akaniambia huku akitabasamu.
“Bahati mbaya hatukuwa
tumeulizana majina. Lakini
natumaini ni mgeni wako”
“Sawa. Mimi naitwa Maimuna.
Wewe unaitwa nani?”
“Mimi naitwa Martin”
“Nimefurahi kukufahamu, karibu
nyumbani”
Nikafuatana na yule msichana
kuelekea kule alikotoka.
Ingawa kulikuwa na giza, sura ya
yule msichana haikuwa ngeni
machoni kwangu. Nilikumbuka
kwamba niliwahi kumuona mahali
fulani pale pale Tanga lakini
sikuweza kukumbuka vizuri
nilimuona mahali gani na sikutaka
kumuuliza.
“Maimuna unaishi na nani?”
“Naishi na mama yangu”
“Ndiyo mmejenga huku?”
“Ndiyo tulikopata kiwanja”
“Lakini baada ya muda si mrefu
kutakuwa ni mji”
“Karibuni eneo lote limeshapimwa
isipokuwa watu wenyewe
hawajaanza kujenga. Wengine
wameanza lakini wanakwenda
taratibu”
“Nyinyi mmeshakamilisha nyumba
yenu?”
“Bado kidogo. Lakini tumeamua
kuhamia hivyo hivyo. Si unajua
adha ya nyumba za kupanga?”
“Ninaijua. Mmefanya uamuzi mzuri.
Mtakamilisha kidogo kidogo
wenyewe mkiwemo ndani”
“Bora tumepiga bati na tunaweza
kukaa, mambo mengine yatafuata.
Hatunaharaka”
Tukatokea mbele ya nyumba moja
kama boma lakini lilikuwa
limepigwa bati. Ilikuwa
imezungukwa na miti ya
mikoroshi.
“Hapa ndio nyumbani” Msichana
akaniambia na kuongeza.
“Karibu ndani”
Alikuwa ametangulia kwenye
mlango akausukuma na kuingia
ndani.
“Karibu” akaniambia.
Nikamfuata. Tulitokea kwenye
chumba kama sebule. Hakikuwa
kimesakafiwa na hata kuta za
chumba hicho hazikuwa
zimepigwa lipu. Juu kulikuwa wazi.
Hakukuwa na dari.
Sebule yenyewe ilikuwa
shaghalabaghala. Kulikuwa na
makochi mawili yaliyokuwa
yamechakaa na meza moja. Taa ya
fanusi ilikuwa imening’inizwa
katikati ya chumba hicho.
“Karibu ukae” msichana
akaniambia.
Nilikaa kwenye kochi mojawapo.
Nikimlinganisha msichana huyo na
ile nyumba vilikuwa ni vitu viwili
tofauti. Msichana alikuwa mzuri na
mrembo kuliko maelezo lakini
nyumba aliyokuwa akiishi ilikuwa
inatisha.
Lakini sikujali. Nilikuwa nimevutika
na yule msichana. Nilijiambia
anafaa hata kumuoa.
Msichana aliongeza mwanga wa ile
taa ya fanusi kisha akaniambia.
“Nisubiri kidogo”
Alielekea uani.
Nikamsubiri. Hapo hapo simu
yangu ikaanza kuita. Nikaitoa
mfukoni na kuona namba ya
kachero mwenzangu ambaye
nyumba zetu zilikuwa jirani.
“Vipi John…?” nikamuuliza mara tu
nilipopokea ile simu.
“Umepata taarifa yoyote kumhusu
Sajenti Erick?” Sauti ya John
ikaniuliza.
“Sijapata taarifa yoyote”
“Nimesikia Sajenti hakuripoti leo
kazini na mke wake amekwenda
kulalamika kituoni usiku huu kuwa
mume wake hajamuona tangu
asubuhi na hajulikani aliko”
“Niko mbali kidogo. Nikirudi
nyumbani tutazungumza”
“Sawa.
Endelea kufuatilia hadithi hii

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.