Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 12

Sote tukasimama. Kila polisi
akachukua bunduki yake.
Tulishindwa hata kujibu, tukawa
tunatazamana.
“Vipi jamani, mbona mmelala
hapa” Inspekta Amour akatuuliza
tena.
Polisi mmoja akaeleza
kilichotutokea. Polisi hao waliokuja
wakashangaa.
Waliusogelea mwili wa Sajenti Erick
na kuutazama.
“Huyu ndiye Sajenti Erick” Amour
akasema baada ya kuutazama
mwili huo. Akaongeza.
“Sasa nini kilitokea?”
“Ni miujiza mitupu” nilijibu mimi.
“Hiyo nyumba imetowekaje?”
“Hatujui. Muda huu tunazinduka
tunaona nyumba haipo”
“Ilikuwa kwa wapi”
“Sisi tulikuwa uani mwa hiyo
nyumba. Lile gari tulilokuja nalo
lilikuwa mbele ya nyumba” polisi
mwingine alijibu.
SASA ENDELEA
“Kwa hiyo nyumba ilikuwa hapa
katikati?”
“Ndiyo. Ilikuwa kati ya sisi na lile
gari” nikajibu.
“Sasa wale watu mnaosema
mliwaona, wako wapi?”
“Hawapo tena, tumezinduka
hatuwaoni” koplo akajibu yeye.
“Walikuwa ni watu wa aina gani?”
“Wale si watu, wale ni majini”
nikasema na kuongeza.
“Wale ndio wamemuua Sajenti
Erick. Yule mwanamke ndiye
tuliyemkamata siku ile kwa
tuhuma za kukutwa na madawa ya
kulevya”
“Lakini yule mwanamke alikufa?”
Amour akasema.
“Kwa kweli tumemuona na ndiye
aliyetupungia mkono, sote
tukapotewa na fahamu” Koplo
akaeleza.
Inspekta Amour akaguna na kutupa
mcho huku na huku.
“Yule binti yake ambaye
aliwatoroka alikuwa pamoja
naye?” akatuuliza tena.
“Walikuwa wote pamoja na
mwenzao mwingine mwanaume”
nikasema.
Nilitupa macho chini nikayaona
yale magazeti ambayo
niliyachukua mle chumbani.
Nikainama na kuyachukua.
“Haya magazeti yana habari ya
yule mwanamke, niliyakuta katika
chumba alichochinjwa Erick”
Nilikunjua gazeti mojawapo
nikampa Inspekta Amour. Amour
alilichukua na kulitazama. Nilimpa
na lile gazeti jingine nalo
akalitazama.
“Itakuwa ni yeye kweli” alisema
baada ya kusoma vile vichwa vya
habari.
Pembeni na eneo hilo kuliwa na
watu wamesimama wakitutazama.
Inspekta Amour alimuita mtu
mmojawapo. Mtu huyo alikuja kwa
uoga akasimama kando ya
Inspekta Amour.
“Wewe ni mwenyeji wa eneo hili?”
Amour alimuuliza.
“Sisi tunaishi kule kando, hapa
tunapita njia tu” Mtu huyo alijibu
huku akionesha kuwa na wasiwasi
“Eti hapa mahali pana nyumba?”
“Hili ni eneo la makaburi tu, hakuna
nyumba” Mtu huyo akamjibu.
“Hujawahi kuona nyumba mahali
hapa jana au juzi?”
“Sijawahi kuona nyumba”
“Sisi tulikuta nyumba tulipokuja
usiku” Koplo akasema.
“Eneo hili ni la makaburi tu” Yule
mtu alisisitiza.
“Kwani jana usiku ulifika hapa?”
Amour aliendelea kumuuliza.
“Jana sikuwahi kufika, nilipita leo
alfajiri nikaona hawa polsi
wamelala hapa, nikaona na ule
mwili umekatwa kichwa…”
Alionesha mwili wa Sajenti Erick.
“Nani aliyepiga simu polisi?’
“Ni mimi. Nilipiga simu baada ya
kuwaona hawa polisi wamelala
hapa na pia ni baada ya kuona mtu
aliyekatwa kichwa”
Inspekta Amour akatutazama.
“Huu ni mkasa mzito, huyu mtu
tutamchukua kwa ajili ya ushahidi.
Sasa tukibebe hiki kiwiliwili
tukiingize kwenye gari”
Baada ya Inspekta Amour
kutuambia hivyo tulikibeba kile
kiwiliwili cha Sajenti Erick na
kukiingiza kwenye gari
tuliyokwenda nayo usiku.
“Tutarudi tena kwa ajili ya kulipiga
picha hili eneo” Inspekta Amour
akatuambia na kumuomba yule
mtu aliyemuita tuende naye polisi
ili akaandikishe maelezo yake na
kisha angerudishwa kwa gari la
polisi.
Baada ya hapo sote tulipanda
kwenye magari tukaondoka. Kwa
mbali nilihisi kichwa kikiniuma na
ile hofu ya usiku bado ilikuwa
ikitambaa kwenye mishipa yangu.
Nilijua nilipata hali hiyo kutokana
na kutolala usiku kucha pamoja na
lile taharuki la usiku. Lazima
kichwa kiume na lazima mwili
usisimke kwa hofu.
Tulifika kituo cha polisi tukashuka
kwenye gari. Tulimkuta kamanda
wa polisi na afisa upelelezi
wakitusubiri. Inspekta Amour
alikuwa amewapigia simu tukiwa
ndani ya gari.
Mara tu tuliposhuka kwenye gari,
maafisa hao walisogea kenye gari
lililokuwa na kiwiliwili cha Sajenti
Erick na kukitazama.
“Kichwa chake kiko wapi?”
Kamanda wa polisi akauliza.
“Kichwa chake hakikupatikana”
Inspekta Amour alimjibu.
Kamanda wa polisi akakunja uso.
“Kwani ilikuwaje? Hebu njoo huku
ndani utueleze”
“Martin twende” Inspekta
akaniambia.
Tukaingia ndani ya kituo. Kamanda
wa polisi alituita kwenye ofisi ya
mkuu wa kituo. Yeye na afisa
upelelezi walikaa. Sisi tukawa
wima.
“Hili tukio ni kubwa hebu tupeni
maelezo, nini kilitokea?” Kamanda
wa polisi akatuambia.
Inspekta Amour alieleza kwa
upande wake. Alieleza
nilivyompigia simu saa tisa usiku
na kuomba msaada wa polisi.
“Alituambia yuko Magomeni na
kwamba alitoroka kutoka katika
nyumba moja ambako aliukuta
mwili wa Sajenti Erick umekatwa
kichwa. Na kwamba yeye
mwenyewe pia amenusurika
kukatwa kichwa na bado hayuko
salama.
“Mimi baada ya kupata habari hii
nilipata hofu kidogo nikatuma gari
na askari sita muda ule ule. Ukapita
muda wa kama nusu saa hivi
Martin akanipigia simu tena
akaniambia lile gari la polisi
limempita, hawakumuona.
Nikawapigia kuwajulisha kuwa
wamempita Martin, warudi nyuma”
“Baada ya hapo kukawa kimya.
Nilijaribu kupiga simu tena
kuwaulizia lakini simu ikawa
haipokelewi. Ilipokuwa inakaribia
kuwa asubuhi mtu mmoja
alitupigia simu akatuambia
ameona polisi wamelala juu ya
makaburi na kuna mtu mmoja
amekatwa kichwa.
“Hapo nilichukua askari na gari na
kuelekea eneo la tukio.
Tulizunguka sana hadi tukafika
katika eneo hilo. Tuliwakuta askari
wamelala kwenye eneo la
makaburi na kiwiliwili cha Sajenti
Erick kipo hapo hapo”
Inspekta Amour aliendelea kueleza
jinsi walivyotuona tukizinduka na
kutuhoji maswali na sisi tukaeleza
kilichotutokea.
Je nini kitafuata? Usikose

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.