Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 11

Mwili na kichwa vimeondolewa.
Nafikiri vimezikwa uani”
nikaongezea maelezo.
“Tumekuta makaburi uani!” Polisi
mwingine akasema.
“”Kwenye hivi vyumba vingine
hamkukuta watu?” Koplo akauliza.
“Hakuna mtu humu ndani. Hii
nyumba iko tupu”
“Hebu twendeni tukayaone hayo
makaburi”
Tukaenda uani. Lile kaburi
nililoliona likichimbwa na yule
mwanamke lilikuwa limefukiwa.
Pembeni yake kulichimbwa kaburi
jingine lililokuwa wazi. Shepe
lilikuwa limeachwa kwenye chuguu
ya mchanga.
“Hili kaburi lililofukiwa ndilo
nililokuta linachimbwa. Bila shaka
mwili wa Sajenti Erick umezikwa
hapa” nikawambia wenzangu.
“Tulifukue tuone ndani” Koplo
akasema.
Lilikuwa wazo zuri.
“Lakini tusitumie hili shepe.
Tutaharibu alama za vidole za
aliyekuwa amelishika” Koplo
akatukumbusha.
“Tunaweza kulifukua hata kwa
mikono. Mchanga wenyewe bado
uko laini” nikawambia.
Bila kujua hatari ambayo ilikuwa
inatukabili, tulianza kulifukua
kaburi hilo kwa mikono.
SASA ENDELEA
Polisi watano nikiwemo na mimi
tuliendelea kulifukua kaburi hilo
kwa mikono. Koplo wetu alikuwa
amesimama na bunduki kuweka
ulinzi. Tulilifukua kaburi hilo hadi
likawa shimo, tukaingia ndani na
kuendelea kufukua.
Wakati tukiendelea kufukua huku
tukimwaga mchanga kwa juu
niliona kiatu cheusi, nikakishika na
kukivuta. Nikaona nimevuta mguu.
“Jamani nimeshika mguu!”
nikawambia wenzangu.
“Ni kweli hapa pamezikwa mtu,
hebu tufukue zaidi” Polisi mmoja
akatuambia.
Tukaendelea kufukua na hatimaye
kuupata mwili kamili usio na
kichwa. Mara moja niligundua
kuwa mwili huo ulikuwa wa Sajenti
Erick na ndio ule uliokuwa
ukining’inia kule chumbani..
“Huu hapa mwili wa Sajenti Erick”
nikawambia wenzangu ambao
walikuwa wameshituka na
kushikwa na mshangao.
“Kichwa chake kiko wapi?” Koplo
akauliza.
“Kichwa hakipo, nadhani
hawakukizika lakini nilikiona
kwenye lile boksi” nikasema.
“Sasa tutauthibitishaje kuwa ni
mwili wa Erick?” Koplo akauliza.
“Lakini unaonekana ni mwili wake
kweli, hili shati ndilo alilokuwa
amevaa jana” Polisi mmoja
akasema.
“Utoeni, tuuangalie vizuri” Koplo
akatuambia.
Tukaubeba na kuuweka juu ya
kaburi.
Koplo akautazama na kutuambia.
“Hata mimi naona ni Sajenti Erick,
hivi viatu ni vya kipolisi. Ngoja
nimfahamishe Inspekta aliyeko
kwenye zamu”
Kiplo alitoa simu akampigia
Inspekta aliyekuwa ameshika zamu
ya usiku ya kuongoza kituo.
“Afande tumefika hapa mahali,
tumeonana na Martin na
tumeukuta mwili wa Sajenti Erick
umezikwa lakini hauna kichwa”
Koplo huyo akazungumza kwenye
simu baada ya simu yake
kupokelewa.
“Hilo kaburi alilozikiwa liko wapi?”
Sauti kutoka upande wa pili wa
simu ikamuuliza.
“Liko uani mwa hii nyumba
tulioingia”
“Mmekamata watu wangapi humo
ndani?”
“Hatukukuta mtu yeyote”
Wakati Koplo huyo akisema hivyo
tulisikia mlango wa mbele wa
nyumba hiyo ukifunguliwa.
Tukamuona yule mwanamke na
binti yake Maimuna pamoja na yule
jini mwanaume wakiingia.
Maimuna na yule jini mwanaume
walikuwa wameshika mapanga.
Polisi wote waliokuwa hapo
walishituka. Walishituka si kwa
sababu tu ya kuwaona viumbe hao,
bali walishituka kwa kuona
maumbile waliyokuwa nayo.
Walikuwa na maumbile ya kijini
huku miguu yao ikiwa na kwato
nyeusi kama kwato za punda!
Koplo aliyekuwa akiongea kwenye
simu alikatiza mazungumzo yake
akaitia simu mfukoni na kuinua
bunduki. Polisi wengine pia
waliinua bunduki zao
kuwaelekezea majini hao.
“Majini wenyewe ndio hao
wanaokuja” nikawambia polisi hao
kwa mshituko. Kwa vile nilikuwa
nyuma nilisimama pale pale
nilipokuwa ili nijikinge kwa
wenzangu waliokuwa na bunduki.
“Simameni hapo hapo!” Koplo
aliwambia majini hao kwa sauti ya
amri.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio.
Kwanza sikuziamini bunduki hizo
za polisi kama zingeweza
kuwatiisha majini hao lakini kwa
vile tulikuwa wengi nilipata
matumaini kidogo.
Majini hao hawakusimama,
waliendelea kuja uani kama vile
hawakusikia walichoambiwa.
“Nimewambia simameni hapo
hapo!” Koplo aliwaamuru tena
akiwa amewaelekezea bunduki.
“Afande tuwababue risasi kama
hawasikii” Polisi mmoja
akamwambia koplo huyo kama
kuwatisha majini hao.
“Nyinyi ni kina nani?” Maimuna
akauliza kwa sauti ya ukali huku
akiwatangulia wenzake.
“Sisi ni polisi” Koplo alimjibu.
Walikuwa wameshafika kwenye
mlango wa uani. Sasa walikuwa
wanavuka kizingiti ili watoke uani.
Koplo akafyatua risasi juu.
“Mtakufa nyote, simameni na
tupeni mapanga yenu!”
akawambia kwa sauti kali.
Yule mwanamke aliinua mkono na
kufanya kama anampiga kibao
koplo huyo lakini akiwa yuko mbali
naye. Hapo hapo koplo aliachia
bunduki akaanguka chini.
Hakuinuka tena. Mwanamke huyo
akageukia upande wetu akafanya
vile vile kwa polisi mwingine
ambaye naye alianguka.
Akaendelea kufanya hivyo hivyo
kwa kila polisi. Wote walianguka
na kila aliyeanguka hakuinuka
tena. Mimi nilikuwa wa mwisho.
Alinipitishia mkono kama
ananipiga kibao nikaona kama
dunia inazunguka. Macho yangu
yakafunga kiza. Nikaanguka hapo
hapo na kupoteza fahamu.
Nilipokuja kuzinduka kulikuwa
kumekucha. Kwanza nilianza kuona
miale ya jua ikipiga kwenye macho
yangu. Nikayafumba kisha
nikayafumbua tena. Nilikuwa
nikijiuliza niko wapi. Sikuweza
kuelewa mara moja. Pia macho
yangu hayakuweza kuona sawa
sawa kutokana na miale ya jua
iliyokuwa ikinipiga usoni.
Nikatulia na kuwaza. Nikakumbuka
kilichotokea. Nikainuka kwa haraka
na kuketi. Nilikuwa nimelala
kwenye tuta la mchanga wa kaburi
mahali palepale nilipoanguka.
Niliwaona polisi wenzangu
waliokuwa wamelala kama
nilivyokuwa nimelala mimi. Kila
mmoja alikuwa sehemu yake,
bunduki yake ikiwa pembeni.
Wakati ule nainuka, polisi hao nao
walianza kuinuka mmoja mmoja.
Walikuwa wamezinduka kama
mimi baada ya kupotewa na
fahamu kwa muda ambao
hatukuujua.
Jambo la ajabu tuliloliona ni kuwa
ile nyumba ya Maimuna haikuwepo
tena. Eneo lote lilikuwa makaburi
matupu. Lile kaburi la Sajenti Erick
ambalo tulilifukua lilikuwepo na
mwili wake ulikuwa juu ya kaburi
hilo kama tulivyouweka.
Gari la polisi tulilokwenda nalo
mahali hapo lilikuwepo. Pia
kulikuwa na gari jingine
lililokwenda na polisi wengine.
Polisi hao tuliwaona wamesimama
wakitutazama.
Kila mmoja wetu aliyeinuka
alikuwa akishangaa. Alishangaa
kwa jinsi tulivyokuwa tumepotewa
na fahamu na alishangaa kuona ile
nyumba haikuwepo tena na badala
yake kulikuwa na makaburi
matupu.
“Vipi?” Inspekta Amour ambaye
alikuwa mmoja wa polisi waliofika
alituuliza kwa mshangao.
Je nini kitatokea?

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.