Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 14

Kamanda akanyamaza na
kututazama. Kikapita kimya kifupi
kabla ya kukitanzua kimya hicho.
“Sasa andikisha maelezo yake,
yatawekwa kwenye faili la
marehemu pamoja na maelezo
yenu nyote” Kamanda
akamwambia Inspekta na
kunigeukia mimi.
“Wewe utatupeleka katika hilo
eneo, tutachukua mpiga picha”
akaniambia.
Wakati Inspekta anachukua
maelezo ya yule mwananchi,
kamanda wa polisi na afisa
upelelezi walitoka nje ya kituo
wakakikagua tena kiwiliwili cha
Sajenti Erick kabla ya kuamuru
kipelekwe hospitali kwa uchunguzi
zaidi.
Baada ya hapo aliitwa mpiga picha
wa polisi. Dakika chache baadaye
kamanda wa polisi, afisa upelelezi,
mpiga picha wa polisi na mimi
tulikuwa kwenye gari tukielekea
katika eneo lilipotokea tukio.
Nikiwa ndani ya gari nilikuwa
nimeinamisha kichwa changu kwa
mawazo. Tukio hilo lilikuwa
limenitia fadhaa sana na sikujua
hatima yake ingekuwa nini.
Hofu yangu ilikuwa kuzuiwa likizo
yangu ambayo ningeianza siku
mbili tu kutoka siku ile.
SASA ENDELEA
Tulipofika katika lile eneo tulishuka
kwenye gari, nikawaonesha
maafande wangu mahali ilipokuwa
ile nyumba.
“Nyumba ilikuwa hapa”
niliwambia.
“Kwa sasa ndiyo imeyayuka?”
Kamanda akauliza.
“Ni kama imeyayuka afande kwa
maana tulipozinduka hatukuiona
tena”
“Na hilo kaburi lililokuwa na mwili
wa marehemu Erick ni lipi?”
Nikawaonesha kaburi hilo ambalo
lilikuwa wazi.
“Ni hili hapa”
Kamanda akamwambia mpiga
picha wa polisi apige picha eneo
hilo.
“Hili kaburi lilioko wazi utalipiga
picha peke yake” aliendelea
kumueleza.
Wakati mpiga picha huyo
akiendelea kufyatua picha., afisa
upelelezi alimwambia.
“Na hii sehemu inayodaiwa ilikuwa
nyumba usisahau kuipiga picha.
Jaribu kupiga picha nyingi zaidi
kwa sehemu tofautu tofauti”
Tuliwa tumesimama katika eneo
hilo huku kamanda wa polisi
akiendelea kunihoji na picha
zikiendelea kupigwa, watu
mmojammoja walianza kufika na
kutuangalia wakiwa wamesimama
kwa mbali.
Afisa upelelezi aliwaita wakasogea
karibu.
“Nyinyi ni wenyeji wa eneo hili?”
akawauliza.
“Ndio ni wenyeji wa eneo hili”
Kijana mmoja akamjibu.
“Nini kilitokea asubuhi hapa?”
“Palikuwa na polisi waliokuwa
wamelala juu ya makaburi”
“Wewe uliwaona?”
“Watu waliokuwa wakipita njia
wote waliwaona”
“Na labda mlijua polisi hao walilala
juu ya makaburi kwa sababu ya
nini?”
“Hatukujua lakini polisi wengine
walifika asubuhi wakawaona”
“Eti hili eneo lina historia gani?”
“Historia ya namna gani?”
“Inasemekana kuna miujiza
inatokea katika eneo hili ni kweli?
“Ni kweli. Siku nyingine ukipita
usiku hapa unakuta mambo ya
ajabu”
“Kama mambo gani?”
“Unaweza kukuta watu wamekaa
wanasoma wamevaa nguo nyepe
tupu au unaweza kukuta
mwanamke mrefu ananyonyesha
mtoto wake”
“Sasa nyinyi wenyeji wa hapa
mnayachukuliaje matukio kama
hayo?”
“Hapa mahali kwa kweli kuna
majini. Wale polisi tuliowakuta
wamelala hapa asubuhi bila shaka
walikumbwa na majini hao”
Mwanamke mmoja aliyekuwa
akisikiliza mazungumzo hayo
aliingilia.
“Pana jini anaitwa Maimuna na
mama yake anaitwa Fatuma. Kuna
siku wanaonekana lakini
hawadhuru mtu”
“Hao majini wanapatikana kwa
wapi?”
“Eneo lao ndilo hili hapa lakini
huwezi kuwaona mpaka usiku”
“Usiku ndio wanaonekana?”
“Mara moja moja wanaonekana”
“Sawa. Asante sana”
Afisa upelelezi akamgeukia
kamanda wa polisi.
“Kinachonishangaza mimi ni kuwa
maelezo ya polisi waliokuja huku ni
kwamba yule mwanamke
waliyemuona ni yule aliyekamatwa
na kete za madawa ya kulevya na
kufia mahabusi, sasa swali
ninalojiuliza muda wote je majini
wanafanya biashara ya madawa ya
kulevya?”
“Au si majini ni watu?” Kamanda
naye akauliza swali lake.
“Hapana ni majini kama
wanavyosema hawa wenyeji
wenyewe. Huyo Maimuna ndiye
yule msichana niliyewaeleza na
yule mwanamke alituambia jina
lake anaitwa Fatuma kama
alivyotueleza huyu msichana hapa”
nikasema.
“Kwa hiyo siku ile nyinyi mlikamata
majini?” Kamanda aliniuliza.
“Ndio, wale walikuwa majini”
nikasisitiza.
“Majini pia wanafanya biashara ya
madawa ya kulevya?’
Hapo sikuwa na jibu kwa sababu
yale madawa ya kulevya, Sajenti
Erick aliwabambikia tu.
“Itabidi tufanye uchunguzi wa
kuthibitisha kama ni kweli hao
majini ndio walikuwa wakazi wa
ile nyumba ya barabara ya nane
alipokamatwa yule mwanamke”
afisa upelelezi akasema.
“Sasa suala la msingi ni kutafuta ile
nyumba ni ya nani na kama
tutakuta watu mle ndani wahojiwe
ili watoe maelezo” Kamanda
akaongeza.
“Sisi tunachofahamu ni kuwa
wanaojenga nyumba au
kupangisha ni watu. Sasa kama
majini pia wanamiliki nyumba au
kupangisha tutakwenda kujua
vizuri” afisa upelelezi akasema.
Baada ya hapo tulirudi kwenye gari
tukaondoka. Kichwa changu
kilikuwa kimevurugika sana. Ile
kesi ilikuwa kama imenilemelea
mimi. Hoja za maafande wangu
zilikuwa zikinitibua mtima. Nikahisi
kama vile mwisho wa siku
nitakamatwa na kushitakiwa mimi.
Nilikuwa na hamu ya kuwaona
wazazi wangu na ndugu zangu
huko kwetu Kagera lakini likizo
yangu ilikuwa kwenye hatari ya
kufutwa kutokana na uchunguzi
huo.
Sikudhani kama polisi
wangeniruhusu niende likizo
wakati kulikuwa na tukio la
uchunguzi kama lile ambalo
lilikuwa linanihusu sana.
Kwa kweli nilifikia mahali nilijuta
kutaka kuanzisha uhusiano na yule
msichana ambaye sikuwa
nikimfahamu. Matokeo yake ndio
hayo ya kukumbwa na mkasa
ulioyatatanisha maisha yangu.
Nilijua kuwa kama polisi
watashindwa kuyathibitisha
maelezo yangu watanihusisha
mimi na mauaji ya Sajenti Erick. Na
kama nitahusishwa na mauaji hayo
ni wazi kuwa nitashitakiwa mimi
kwa kufunguliwa kesi ya mauaji.
Je nini kitaendelea? Usikose
kufuatilia

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.