Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 08

Leo nimekwisha!” nikajiambia.
Nilikuwa sina pa kukimbilia. Lakini
nilikwishatambua kila kitu.
Sikujua niliwezaje kuwasiliana na
yule msichana hadi nikafika katika
nyumba ile ya mauti! Kusema kweli
nilijipeleka mwenyewe!
Kwa vyovyote vile, nilijiambia,
nyumba ile haikuwa ya binaadamu
wa kawaida. Yule bibi alikuwa jini!
Na kama alikuwa jini, niliendelea
kujiambia, sitaweza kunusurika mle
ndani.
Licha ya kutoka pale uani, yule bibi
hakushituka. Aliendelea kuchimba
lile shimo kwa bidii.
Hakuna binaadamu yeyote
anayekubali kufa kirahisi,
nikageuka haraka na kurudi
nilikotoka. Wakati nafika kwenye
mlango wa mbele, mlango huo
ulikuwa unafunguliwa. Nilijificha
nyuma ya mlango. Akaingia yule
msichana.
Na yeye alikuwa uchi na alikuwa na
umbile sawa na lile la mama yake.
Alikuwa amejaa manyoya mwili
mzima na miguu yake ilikuwa ya
kwato nyeusi. Mkononi alikuwa
ameshika upanga.
Mwenzake alikuwa mwanaume. Na
yeye alikuwa kama walivyokuwa
wenzake. Hapo nikagundua kuwa
yule mama na binti yake
waliokuwa wakiuza vitu vya
dhahabu, walikuwa ni majini lakini
watu hawakuwa wakijua.
SASA ENDELEA
Ule upanga aliokuwa ameushika
Maimuna ulikuwa wa nini?
Nikajiuliza.
Lakini jibu lilikuwa wazi kuwa
upanga huo ulikuwa ni kwa ajili ya
kuchinja kichwa changu. Bila shaka
ndio uliotumika kumchinja Sajenti
Erick.
Usiku huo ulikuwa wa balaa
kwangu. Nilijuta kulaimisha
mawasiliano na yule msichana hadi
yakanikuta yaliyonikuta. Lakini
nilihisi kukutana tena na majini hao
ilikuwa ni mipango yao ya
kutukomoa kama walivyomkomoa
Sajenti Erick kutokana na ile
dhambi tuliyowafanyia.
Kosa langu ni kuwa nilijiingiza
kichwa kichwa mara tu Maimuna
aliponitumia meseji aliyodai kuwa
haikuwa yangu bali alikosea
namba. Ilikuwa tamaa yangu ya
wasichana iliyopelekea nifike
mahali hapo pa mauti.
Maimuna na mwenzake
walipoingia hawakuufunga ule
mlango wa nje. Kama
wangeufunga wangeniona.
“Yuko wapi?” Maimuna akauliza
alipoona sikuwepo mahali ambapo
nilikuwa nimelala. Akakimbilia
uani. Mwenzake aliyekuwa naye
akamfuata.
Hapo ndipo nilipopata upenyo wa
kutoka. Nilipotoka nje nilianza
kukimbia. Jambo lililonishangaza ni
kuwa nilijiona niko kwenye msitu
wa kutisha. Nilikuwa najikimbilia
ovyo bila kujua nilikuwa
ninakwenda wapi.
Nikatoa simu yangu mfukoni na
kuwapigia polisi wenzangu ili
nipate msaada. Wakati napiga simu
nilikuwa nakimbia. Simu
ilipokelewa. Aliyepokea alikuwa
mwanamke. Nikamwambia.
“Mimi ni Martin Lazaro wa CID
nimepatwa na matatizo, naomba
msaada wenu”
“Mimi ni Maimuna. Uko wapi
Martin, nakutafuta?” Sauti
ikaniuliza kutoka simu ya upande
wa pili. Mara moja niliitambua sauti
ya Maimuna.
Nikaikata simu haraka kwa kuona
nilikuwa nimekosea namba na
kumpigia yule msichana muuaji
niliyekuwa namkimbia.
Nikasimama na kuiangalia kwa
makini namba ya polisi kisha
nikaipiga. Nilikuwa nimesimama.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio na
nilikuwa nahema kama niliyekuwa
nafukuzwa.
Simu ikapokelewa tena. Kabla ya
kusema chochote nikaisikia tena
sauti ya Maimuna ikiniuliza.
“Uko wapi?”
Moyo ukanilipuka kwa hofu.
Nikaitazama ile namba. Nikaona ni
namba ya polisi lakini aliyepokea
alikuwa Maimuna. Nikaamini kuwa
wale walikuwa majini kweli.
Nikakata simu na kuendelea
kukimbia. Simu ikawa inapigwa.
Nikasimama na kutazama namba
iliyokuwa inapiga, nikaona namba
ya polisi.
Nikaipokea haraka.
“Jamani nina matatizo, nikipiga
simu inakwenda kwingine…”
“Inakwenda wapi?” Sauti
iliyoniuliza ilikuwa ya Maimuna.
“Wewe nani?” nikamuuliza kwa
kutaharuki.
“Mimi Maimuna umenisahau mara
moja hii, wakati tulikuwa wote
hapa nyumbani…”
Nikakata ile simu na kuendelea
kukimbia. Kutahamaki nikajiona
nimetokea mbele ya ile nyumba ya
Maimuna.
Nilikuwa nakimbia lakini nilipiga
breki ya ghafla, nikaitazama ile
nyumba iliyokuwa mbele yangu.
Nilihakikisha kuwa ilikuwa ndio ile
ile nyumba ya Maimuna na mahali
palikuwa pale pale. Kwa maneno
mengine ni kwamba nilikuwa
nimerudi hapo hapo.
Mlango ulikuwa umefungwa,
nikaona unafunguliwa. Sikujua nani
angetoka, nikageuka na kuanza
tena kukimbia. Sasa nilikuwa kama
mwendawazimu niliyekuwa
nikijikimbilia ovyo.
Wakati ninakuja katika eneo lile
hakukuwa na msitu. Kulikuwa na
vichaka tu na miti michache ya
mikoroshi. Sasa niliona ajabu kuona
msitu wa kutisha. Sikuweza kujua
jinsi msitu huo ulivyotokea.
Simu yangu ilkuwa inaita lakini
sikushughulika nayo tena,
niliendelea kukimbia tu. Nia yangu
ilkuwa kutokea katika barabara au
njia ya watembea kwa miguu lakini
sikuona njia wala barabara.
Ghafla niliona nyumba kwa mbali.
Ilikuwa inawaka taa kwa nje,
nikakimbilia kwenye nyumba hiyo
ili kuomba msaada. Nilipofika
niligonga mlango.
“Jamani naomba msaada…jamani
naomba msaada” nikasema huku
nikiendelea kugonga.
Baada ya muda kidogo mlango
ukafunguliwa.
“Karibu” Bibi mmoja aliyekuwa
amejitanda shuka nyeupe
akanikaribisha.
Nikamueleza ule mkasa ulionifika.
Nilipomaliza kumueleza
akapandisha juu gauni lake na
kuniuliza.
“Hao watu unaosema wana kwato,
kwato zao ni kama hizi?”
alinionesha miguu yake.
Nilipoitazama nikaiona ina kwato
kama zile za kina Maimuna!
Nikashituka na kumtazama yule
bibi usoni. Sasa nikamuona vizuri.
Alikuwa ndiye yule aliyekuwa
akichimba kaburi kule uani kwa
Maimuna.
“Eh! Amefikaje huku!” nikajiuliza
kabla ya kugeuka nyuma na
kuanza tena kukimbia.
“Mbona unakimbia?” akaniuliza.
Sikumjibu, niliendelea kukimbia.
“We kijana hebu njoo…” Yule bibi
alinipigia kelele.
Nikageka na kumtazama. Alikuwa
ametoka nje akiniangalia.
Nikajipoteza kwenye msitu.
Nilikuwa nimechoka na moyo
ulikuwa ukinienda mbio sana.
Nilijua kuwa wakati wowote
ningeweza kuanguka na kuzimia.
Kitisho nilichokipata kilikuwa
kikubwa na kiliutikisa moyo wangu
hasa. Sikuwa mtu wa kuamini
mashetani lakini siku ile niliamini
kuwa mashetani wapo na
wanatisha. Licha ya kujitahidi
kukimbia muda wote nilijua kuwa
nitakufa kwani sikuwa na ujanja
wa kutoka kwenye msitu huo. Ile
hofu peke yake ingweza kuniua.
Hapo nikaanza kumlaumu Sajenti
Erick kwani yeye ndiye aliuleta
mpango ule wa kwenda
kumkamata yule bibi na
kumbambikia kesi ya madawa ya
kulevya.
Je nini kitatokea?

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.