Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 07







Nikairudisha ile simu mfukoni.
Wakati nairudisha ilikuwa kama
ninaizima akili yangu kwani hapo
hapo sikujielewa tena. Sikujua
kama nilipotewa na fahamu au
nilipitiwa na usingizi wa ghafla.
Sikuweza kujua.
Nilipozinduka nilijiona nimechoka,
kitu ambacho kilinipa dalili kuwa
nililala kwa muda mrefu pale
kwenye kochi. Nikatazama saa
yangu na kuona ilikuwa saa tisa
usiku. Nikataharuki. Mwenyeji
wangu hakuwepo. Nilikuwa bado
niko peke yangu.
Nikajiuliza Maimuna alikuwa
amekwenda wapi tangu muda ule.
Nikanyanyuka na kuanza
kumtafuta mwenyeji wangu.
Niliingia ukumbini nikaita
“Maimuna!”
Lakini sikupata jibu. Nikasukuma
mlango wa chumba cha kwanza
ambao ulikuwa wazi.
Nikachungulia ndani. Chumba
kilikuwa kitupu lakini kulikuwa na
boksi kubwa lililowekwa nyuma ya
mlango.
Nilichungulia ndani ya lile boksi
nikaona kitu kilichonishitua.
Nikaingia mle chumbani na
kutazama vizuri. Ndani ya lile boksi
niliona kichwa cha binaadamu,
tena kilikuwa kichwa cha Sajenti
Erick!
SASA ENDELEA
Kwa kweli nilipatwa na mshituko
mkubwa. Vile ambavyo nilitoka
usingizini nilijihisi kama nilikuwa
kwenye ndoto ya kutisha. Kwa
kutoamini macho yangu
nilikitazama kile kichwa tena na
tena. Akili yangu ilinithibitishia
kuwa sikuwa kwenye ndoto na
nilichokiona ni kichwa cha
binaadamu na ni cha Sajenti Erick!
Nikawa najiuliza Sajenti Erick
alichinjwa muda gani na alichinjwa
na nani na kwanini kichwa chake
kipo pale? Nikakumbuka kwamba
nilipigiwa simu na kachero
mwenzangu aliyenieleza kuhusu
kutoonekana kazini kwa Sajenti
Erick mchana kutwa wa siku ile.
Kile kichwa kwa jinsi
kilivyoonekana hakikuchinjwa
muda mrefu. Jeraha lake lilikuwa
bado bichi na lilikuwa linavuja
damu. Macho ya Sajenti Erick
yalikuwa wazi kuonesha kuwa
wakati anachinjwa alikuwa
ameshituka.
Akili ya kupelelezi ikaanza kunijia.
Nikazungusha macho yangu
kwenye kile chumba. Sikuona
mahali popote palipokuwa na
damu, hali iliyoonesha kuwa
Sajenti Erick hakuchunjwa mle
chumbani.
Wakati nayarudisha macho yangu
kwenye lile boksi nikaona magazeti
kwenye pembe moja ya kile
chumba. Nikaenda kuyatazama.
Yalikuwa magazeti mawili
yaliyowekwa pamoja. Juu ya
magazeti hayo kulikuwa na kete
tatu ambazo nilishuku zilikuwa
kete za kokeni.
Nilizishika na kuzinusa. Kwa vile
nilikuwa na uzoefu na unga huo
haramu niligundua harufu yake.
Ilikuwa ni kokeni. Nikaziweka
kando. Sasa nilishika yale magazeti.
Nilianza kuangalia mojawapo.
Kwenye ukurasa wa mbele
kulikuwa na habari ya ajuza
(kikongwe) aliyekamatwa Tanga na
kete za madawa ya kulevya.
Picha yake ilikuwa imechapwa.
Nilipoitazama nikagundua ilikuwa
ni ya yule mwanamke
tuliyemkamata siku ile mimi na
Sajenti Erick. Kumbe habari zake
zilichapwa kwenye gazeti.
Nikatazama tarehe ya lile gazeti
nikaona ni la siku za nyuma.
Nikashika lile gazeti jingine. Katika
ukurasa wake wa mbele kulikuwa
na habari iliyohusu kifo cha yule
kikongwe ambacho kilitokea katika
mahabusi ya polisi.
Mpaka muda ule nilikuwa sijaelewa
kitu. Nilikuwa nikijiuliza mengi
ambayo hayakuwa na majibu.
Wakati naliweka lile gazeti nikaona
kitone cha damu kikidondoka
kwenye kiganja changu.
Nikashituka na kutazama juu.
Huko juu niliona kitu cha
kushitusha. Niliuona mwili wa
Sajenti Erick usio na kichwa ukiwa
umening’inizwa kwenye miti
iliyopaulia nyumba! Lile jeraha la
kwenye shingo ndilo lililotonesha
tone la damu lililotua kwenye
kiganja changu.
Mwili ule uliunda picha ya kutisha
sana hasa kwa vile mtu mwenyewe
nilikuwa namfahamu. Ujasiri wa
kipolisi niliokuwa nimebaki nao
uliniishia pale pale. Kama
nisingekuwa makini
ningekurupuka na kutoka mbio
kwani hisia zangu zilishanusa hali
ya hatari.
Nilijua kuwa hata mimi maisha
yangu yalikuwa hatarini. Mahali
nilipoingia palikuwa sipo!. Nikainua
hatua ili nitoke katika kile chumba.
Baada ya kupiga hatua mbili
nilikanyaga mahali palipotitia!
Nikajiona natumbukia chini.
Lilikuwa shimo la urefu wa kama
futi nne. Miguu yangu ilipotua chini
nikaona kitu kinanizongazonga
kwenye miguu kikinipandia juu.
Nikajaribu kukishika. Nikaona
nimeshika kichwa cha nyoka!
“Yesu wangu!” nilishituka na
kukivuta juu. Haikuvutika kwani
sehemu yake ya mkia ilikuwa
imenizonga kwenye mguu. Nilitaka
kuwania kupanda juu ya lile shimo
nitoke lakini nilijiambia nikikiacha
kile kichwa nyoka yule atanigonga.
Nikakipeleka kichwa hicho chini ya
mguu mwingine kisha
nikakikanyaga kwa kupiga mguu
wangu chini. Kile kichwa kilipasuka.
Ndipo nilipoweza kutoka kwenye
lile shimo. Nilikuwa nahema kama
niliyekuwa nafukuzwa.
Nilipotoka tu kwenye shimo hilo
nilikwenda ukumbini nikaelekea
kwenye mlango wa nje.
Nilipoushika ili niufungue nikaona
ulifungwa kwa nje. Mlango
haukufunguka!
Nikasikia sauti za watu waliokuwa
wakizungumza huko nje. Sauti ya
mwanaume na mwanamke.
Zilikuwa zikisikika kwa mbali lakini
zilikuwa zikikaribia kwenye ule
mlango. Nikajua ni watu
wanakuja.
Nikatega masikio kuwasikiliza.
“Sasa mama yuko wapi?” Ilikuwa
sauti ya kiume iliyouliza.
“Mama yuko uani, anachimba
kaburi kabisa” Sauti iliyojibu
niliitambua, ilikuwa ni ya yule
msichana aliyenikaribisha mle
ndani.
“Na huyo polisi mwingine
aliyewabambikia kesi yuko wapi?”
Ile sauti ya kiume ikauliza tena.
“Nilimuacha ukumbini amelala, sijui
kama atakuwa ameamka”
“Sasa acha tumshughulikie na yeye
kama mwenzake”
“Mama yangu, nimekwisha!”
nikajiambia niliposikia maneno
hayo. Kumbe tatizo lilikuwa ni ile
kesi tuliyombambikia yule
mwanamke.
Sasa akili yangu ilitanzuka.
Nilimkumbuka yule msichana.
Alikuwa ndiye yule aliyekuwa na
yule mwanamke kwenye ile
nyumba tulipokwenda
kuwakamata. Yule msichana
alikimbia, tukamshikilia mama
yake peke yake.
Kwa hofu kwamba ningeuawa
kama alivyouawa Sajenti Erick,
nilikimbilia kwenye mlango wa
uani. Niliukuta mlango upo wazi,
nikatoka uani ambako kulikuwa
kiza lakini kulikuwa na
mbalamwezi.
Kwenye pembe moja ya ua huo
nilimuona bibi mmoja ameshika
shepe akichimba shimo.
Nilipomuona tu nikakumbuka yale
maneno ya yule msichana
niliyemsikia akisema “Mama yuko
uani, anachimba kaburi kabisa”
Nikajiuliza lilikuwa kaburi langu au
ni la Sajenti Erick? Wakati
namtazama yule bibi
nikamkumbuka. Alikuwa ni yule
mwanamke tuliyemkamata na
kumbambikia kesi ya kumkuta na
madawa ya kulevya.
Jambo ambalo lilinishangaza ni
kuwa mwanamke huyo alikufa
akiwa mahabusi lakini muda ule
nilimuona akiwa hai tena
akionekana akiwa na nguvu za
kutosha.
Kitu ambacho kilikuwa cha ajabu
zaidi ni kuwa bibi huyo alikuwa
uchi wa mnyama na mwili wake
ulikuwa umejaa manyoya meupe
marefu. Nikaiona miguu yake,
ilikuwa na kwato kama miguu ya
punda!
Je nini kitatokea? Usikose
kuendelea na hadithi hii kesho.


No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.