Hakika Yalionikuta Maishani Ni Mengi sehemu ya 10

Maimuna alikuwa ameshika ule
upanga wake akiangaza macho
yake huku na huku. Sikuweza tena
kusubiri, nikatoka mbio. Nilielekea
upande ule lilikoelekea gari la
polisi.
Wakaniona!
“Si yule!” niliisikia sauti ya
Maimuna.
“Twende tumfuate” Sauti ya kiume
nayo ikasikika.
Niliendelea kukimbia. Kila
nilipopiga hatua tatu nilitazama
nyuma. Niliwaona wananifuata.
Hawakuwa wakikimbia lakini
walikuwa wanakuja kwa haraka.
Kwa mbali nikaona mwanga wa
gari linalokuja. Nikazidi kukimbia.
Niliona nikimbie nikiwa katikati ya
barabara ili watu waliomo ndani ya
gari hilo waweze kuniona.
Nikajitokeza katikati ya barabara
huku taa za gari zikinimulika.
Haikutosha kujitokeza katikati ya
barabara. Niliinua mikono yangu
miwili nikawa nalipungia gari hilo
ili kulisimamisha. Niliomba gari hilo
liwe la polisi lililonipita. Kama
halitakuwa gari la polisi
halitasimama. Litanikwepa na
kuendelea na safari yake.
“Jamani simameni, nakufa.. jamani
simameni nakufa!” nilikuwa
nikipiga kelele.
Nyuma yangu Maimuna na
mwenzake walikuwa wakiendelea
kunifuata bila kujali kama kulikuwa
na gari linakuja.
Sikuwa na hakika kama gari hilo
lilikuwa la polisi. Na kama lilikuwa
na polisi sikuwa na hakika kama
wangeweza kupambana na majini
hao waliokuwa na hasira na mimi.
SASA ENDELEA
Gari hilo lilipunguza mwendo na
kusimama katikati ya barabara.
Kama lingeendelea kuja
lingenigonga kwa vile na mimi
nilikuwa katikati ya barabara.
Taa za gari hilo zilikuwa
zikinimulika. Mpaka muda huo
sikujua gari hilo lilikuwa la nani.
Mara tu liliposimama, niliona polisi
wakishuka haraka haraka.
Walikuwa polisi sita waliokuwa na
bunduki. Hapo nikajua kuwa
lilikuwa gari la polisi ambalo
lilinipita mara ya kwanza.
Walikuwa wameshanitambua
wakanifuata haraka haraka.
“Kitu gani Martin?” Polisi mmoja
aliyekuwa na cheo cha Koplo
akaniuliza.
“Nikageuka nyuma ili niwaoneshe
wale majini. Nilishaanza kuwambia.
“Wale majini bado wananifuata…”
Lakini nilisita nilipoona wale majini
hawapo. Walitoweka ghfla nyuma
yangu.
“Kitu gani Martin?” Polisi huyo
aliniuliza tena baada ya
kutonielewa.
Sasa nikawaeleza kwa utulivu
mkasa mzima.
“Sasa wako wapi hao majini?”
Polisi mwingine akaniuliza.
“Wametoweka sasa hivi”
“Una hakika kwamba Sajenti Erick
amechinjwa na umekiona kichwa
chake kiko mbali na mwili wake?”
yule koplo wa polisi akaniuliza.
“Nimekiona kichwa chake kiko
ndani ya boksi na mwili wake
unaning’inia juu”
“Ni sehemu gani?”
“Sehemu yenyewe mmeipita, ni
pale mbele kwenye mbuyu”
Niliwaonesha kwa kidole.
“Ingia kwenye gari twende”
Nilikuwa wa kwanza kujipakia
kwenye gari. Nilikaa kwenye siti
iliyokuwa kando ya dereva. Mwili
wote ulikuwa umenijaa baridi ya
hofu. Baada ya polisi hao kujipakia,
gari likaondoka. Tulipokuwa
tunaukaribia ule mbuyu, polisi
aliyekuwa akiendesha aliniuliza.
“Ni mbuyu ule pale?”
“Ndio ule pale. Kuna njia upande
wa kushoto”
Tulipofika katika eneo lililokuwa na
mbuyu huo, dereva alikata
kushoto. Tukaingia kwenye
vichaka.
“Ni kwa upande gani?”
“Twende tu. Huko mbele kuna njia
inaelekea kulia”
Tulipoifikia njia hiyo inayoelekea
kulia, dereva akaniuliza.
“Njia yenyewe ndio hii?”
“Ndiyo hii, sasa kata kulia. Tutaiona
hiyo nyumba”
Dereva akakata kulia.
“Huku ulifikaje wewe?” Dereva
huyo akaniuliza.
“Ni ushawishi tu wa yule msichana”
nikamjibu.
“Huoni kama kunatisha?”
Nikaguna na kunyamaza kimya.
Muda ule ndio niliona kunatisha.
Wakati ule namfuata yule msichana
sikuona kama kunatisha kiasi kile.
“Yaani sajenti Erick ni marehemu?”
polisi aliyekuwa akiendesha gari
hilo alikuwa bado haamini
niliyowaeleza.
“We twende, utakwenda ona
mwenyewe”
Baada ya mwendo mfupi tukaiona
ile nyumba mbele yetu.
“Nyumba yenyewe ni ile pale”
nikamwambia polisi aliyekuwa
akiendesha.
Akalisimamisha gari mbele ya
nyumba hiyo. Tukashuka. Koplo wa
polisi aliishika vyema bunduki yake
akaenda kubisha mlango. LIcha ya
kubisha kwa sekunde kadhaa
hakukuwa na majibu. Akaupiga
teke mlango huo ambao
ulifunguka.
Mlango ulipofunguka aliwaashiria
polisi wengine wamfuate. Sote
tukaingia ndani. Kila polisi alikuwa
ameielekeza mbele bunduki yake
tayari kukabiliana na tukio lolote
litakalotokea.
Kwa kutumia mwanga ule wa
fanusi ambayo bado ilikuwa
inawaka tuliangaza macho kila
upande. Ile sebule ilikuwa tupu.
Tukaingia ndani zaidi.
Nilimuonesha koplo wa polisi kile
chumba kilichokuwa na kichwa cha
Sajenti Erick pamoja na mwili wake.
Kabla ya kuingia koplo huyo
aliwaashiria polisi wawili kwenda
uani na kumuweka chini ya ulinzi
yeyote watakayemuona.
Aliwambia polisi wengine waingie
katika vumba vingine kwa wakati
mmoja. Ndipo mimi na yeye
tulipoingia katika kile chumba.
Polisi mmoja alikuwa amebaki
ukumbini kmwa ajili ya kuweka
ulinzi.
Tulipoingia humo chumbani
niliutazama ule mwili uliokuwa
ukining’inia, haukuwepo.
Nikalisogelea lile boksi lililokuwa
nyuma ya mlango na kulitazama
ndani. Kile kichwa hakikuwemo
isipokuwa damu iliyokuwa ikivuja
kutoka kwenye kichwa hicho ndio
iliyosambaa ndani ya boksi.
“Kichwa chenyewe kilikuwa humu
lakini kimeondolewa”
nikamwambia koplo huyo.
“Una maana hii damu ilitoka
kwenye kichwa hicho”
“Ndiyo. Kilikuwa kinavuja damu”
“Na ule mwili uliosema ulikuwa
unaning’inia uko wapi?”
“Ulikuwa uking’inia hapa”
Nikamuonesha pale mahali
ambapo chini yake palikuwa na
matone ya damu.
“Ulikuwa unadoda damu, hii hapa
chini”
“Ina maana wameuondoa?” Koplo
akaniuliza. Uso wake ulikuwa
umeshabadilika rangi kwa taharuki.
“Wameuondoa au wameuzika, kwa
sababu yule bibi alikuwa akichimba
kaburi uani”
“Hebu twende na huko”
Koplo alitangulia kutoka. Mimi
niliyachukua yale magazeti
yaliyokuwa yamewekwa pembeni
mwa chumba kisha nikatoka.
Polisi wote tukakutana tena hapo
ukumbini.
“Mmekuta nini?” Polisi mmoja
aktuuliza.
“Kuna damu tu” Koplo alimjibu.
Je nini kitatokea?

No comments

Theme images by konradlew. Powered by Blogger.